WATAKATIFU FILIPO NA YAKOBO MITUME
MASOMO
SOMO: 1Kor.15:1-8
Ndugu zangu, nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama,
na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri; isipokuwa mliamini bure. Kwa maana
naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya
dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama
yanenavyo maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara; baadaye aliwatokea ndugu zaidi
ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala; baadaye akamtokea
Yakobo; tena na mitume wote; na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa
wakati wake.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.19:1-4(K)4
1. Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
Mchana husemezana na mchana,
Usiku hutolea usiku maarifa.
(K) Sauti yao imeenea duniani mwote.
2. Hakuna lugha wala maneno,
Sauti yao haisikilikani.
Sauti yao imeenea duniani mwote,
Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.
Katika hizo ameliwekea jua hema. (K)
SHANGILIO: Yn.14:6,9
Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi njia,
na kweli na uzima, asema Bwana,
Filipo, aliyeniona mimi,
amemweona Baba.
Aleluya.
INJILI: Yn.14:6-14
Yesu alimwambia Tomasi: Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia
ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba, tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. Filipo
akamwambia, Bwana, utuoneshe Baba, yatutosha. Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku
hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuoneshe
Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo
mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. Mnisadiki
ya kwamba mimi ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu
ya kazi zenyewe. Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye
atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. Nanyi mkiomba
lolote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lolote
kwa jina langu, nitalifanya.
MAOMBI
Ndugu zangu wapendwa, Kwa maombezi ya Mitume tumwombe Kristo, Bwana wa Kanisa lake.
1. Uliwaweka mitume kuwa mashahidi wa ufufuko wako na kuwatuma duniani kote waitangaze habari
hii ya furaha: Uwasaidie Baba Mtakatifu J. na maaskofu wote uliowachagua
kuwa mahalifa wa mitumne wako kuliongoza kanisa lako kwa busara na hekima.
2. Uliwaagiza mitume watangaze neno lako kati ya mataifa yote: Uwajaze Roho Mtakatifu wahubiri
wote wa neno lako.
3. Uliweka kanisa lako juu ya msingi wa mitume: Ulifanye Kanisa lako kuwa alama ya umoja na ya
amani kati ya mataifa.
4. Uliwaagiza mitume wawaondolee dhambi wale wote wanaotubu: Uwatie moyo mpya wote wanaoungama
dhambi zao.
Bwana Yesu, unastahili kupokea heshima yote, upokee shukrani na sifa katika Kanisa lako pamoja
na Baba na Roho Mtakatifu sasa na siku zote daima na milele. Amina.