KUONGOKA KWA PAULO MTUME
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: 2Tim.1:12;4:8
Namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake
hata siku ile, yeye aliye mhukukumu mwenye haki.
KOLEKTA:
Ee Mungu, uliufundisha ulimwengu mzima kwa njia ya mahubiri ya mtakatifu Paulo, mtume. Tunakuomba
utujalie sisi tunaoadhimisha leo kuongoka kwake, ili, kwa mifano yake, tutembee kukuelekea wewe na
tuwe mashahidi wa ukweli wako duniani. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na
kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Mdo.22:3-16
Paulo aliwaambia makutano, Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa
katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi nikawa mtu wa
jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi; nikawaudhi watu wa njia hii hata kuwaua,
nikawafunga, nikiwatia gerezani wanaume na wanawake. Kama Kuhani Mkuu naye anishuhudiavyo, na
wazee wa baraza wote pia, ambao nalipokea barua kwao kuwapelekea ndugu wale, nikaenda Dameski,
ili niwalete wale waliokuwa huko hata Yerusalemu, hali wamefungwa, ili waadhibiwe. Ikawa nilipokuwa
nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia
pande zote. Nikaanguka nchi, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi? Nikajibu,
Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi. Na wale waliokuwa
pamoja nami, waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti ya Bwana? Bwana akaniambia, Simama,
uingie Dameski, na huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye. Na nilipokuwa sioni
kwa sababu ya fahari ya nuru ile, nikaongozwa na mikono yao waliokuwa pamoja nami, nikaingia Dameski.
Basi mtu mmoja, Anania, mtauwa kwa kuifuata sheria, aliyeshuhudiwa wema na Wayahudi wote waliokaa
huko, akanijia, akasimama karibu nami akaniambia, Ndugu yangu Sauli, uone. Nikamwinulia macho yangu
saa ile ile. Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule
Mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake. Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu
wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia. Basi sasa unakawilia nini? Simama, ubatizwe, ukaoshe
dhambi zako, ukiliitia jina lake.
Au: Somo: la kuchagua
Mdo.9:1-22
Sauli alizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe
barua za kwenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi; ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake,
awafunge na kuwaleta Yerusalemu. Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula
ikamwangaza kotekote nuru kutoka mbinguni. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli,
Sauli, mbona waniudhi? Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe.
Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda. Na wale watu waliosafiri pamoja
naye wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione mtu. Sauli akainuka katika nchi, na macho yake
yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski. Akawa siku tatu haoni; hali,
wala hanywi. Basi palikuwepo Dameski mwanafunzi jina lake Anania. Bwana akamwambia katika maono,
Anania! Akasema, Mimi hapa, Bwana! Bwana akamwambia, Simama nenda zako katika njia iitwayo Nyofu
ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu aitwaye Sauli, wa Tarso; maana, angalia, anaomba; naye amemwona
mtu, jina lake Anania, akiingia, na kumwekea mikono juu yake, apate kuona tena. Lakini Anania
akajibu, Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu
wako Yerusalemu; hata hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge wote wakuitiao Jina lako.
Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu
mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. Maana nitamwonesha yalivyo mengi yatakayompasa
kuteswa kwa ajili ya Jina langu. Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani, akamwekea mikono akisema,
Ndugu Sauli, Bwana amenituma, Yesu, yeye aliyekutokea katika njia ulioijia, upate kuona tena, ukajazwe
Roho Mtakatifu. Mara vikaanguka machoni pake vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama, akabatizwa,
akala chakula na kupata nguvu.
Akawa huko siku kadha wa kadha pamoja na wanafunzi walioko Dameski. Mara akamhubiri Yesu katika
masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu. Na wote waliosikia wakashangaa, wakasema, Siye huyu
aliyewaharibu walioliitia Jina hili huko Yerusalemu? Na hapa alikuwa amekuja kwa kusudi hilo,
awafunge na kuwapeleka kwa wakuu wa makuhani? Sauli akazidi kuwa hodari, akawatia fadhaa Wayahudi
waliokaa Dameski, akithibitisha ya kuwa huyu ndiye Kristo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.117:1-2
1. Aleluya! Enyi mataifa yote, msifuni Bwana,
enyi watu wote, mhimidini.
(K) Enendeni ulimwenguni mwote,
mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
AU
Aleluya!
2. Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
na uaminifu wa Bwana ni wa milele. (K)
SHANGILIO: Yn.15:16
Aleluya, aleluya,
Niliwachagua ninyi,
nikawaweka mwende mkazae matunda,
na matunda yenu yapate kukaa.
Aleluya.
INJILI: Mk.16:15-18
Yesu alionekana na wale kumi na mmoja, akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri
Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Maana ishara
hizi zitafuatana na hao waaminio, kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;
watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao
juu ya wagonjwa, nao watapata afya.
MAOMBI
Ndugu zangu wapendwa, Kwa maombezi ya Mitume tumwombe Kristo, Bwana wa Kanisa lake.
1. Uliwaweka mitume kuwa mashahidi wa ufufuko wako na kuwatuma duniani kote waitangaze habari hii
ya furaha: Uwasaidie Baba Mtakatifu F. na maaskofu wote uliowachagua kuwa mahalifa wa mitume wako
kuliongoza kanisa lako kwa busara na hekima.
2. Uliwaagiza mitume watangaze neno lako kati ya mataifa yote: Uwajaze Roho Mtakatifu wahubiri wote
wa neno lako.
3. Uliweka kanisa lako juu ya msingi wa mitume: Ulifanye Kanisa lako kuwa alama ya umoja na ya amani
kati ya mataifa.
4. Uliwaagiza mitume wawaondolee dhambi wale wote wanaotubu: Uwatie moyo mpya wote wanaoungama
dhambi zao.
Bwana Yesu, unastahili kupokea heshima yote, upokee shukrani na sifa katika Kanisa lako pamoja na
Baba na Roho Mtakatifu sasa na siku zote daima na milele. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunapoadhimisha mafumbo haya matakatifu, tunakuomba Roho wako atuangaze kwa ile
nuru ya imani, ambayo ilimwangaza daima mtakatifu Paulo, mtume, kwa ajili ya kuutangaza
utukufu wako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
UTANGULIZI wa mitume I.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Yn.1:12
Nina uhai katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana Mungu wetu, sakaramenti tulizopeka ziwashe ule moto wa mapendo ndani yetu, moto
uliowaka ndani ya mtakatifu Paulo, mtume, na ukampa ari ya kuyashughulikia Makanisa yote. Kwa
njia ya Kristo Bwana wetu.