26
Mpango wa kumuua Yesu
(Marko 14:1-2; Luka 22:1-2; Yoh 11:45-53)
1 Yesu alipomaliza kusema hayo yote, aliwaambia wanafunzi wake,
2 âMnajua kwamba baada ya siku mbili tutakuwa na sikukuu ya Pasaka, na Mwana wa Mtu atatolewa ili asulubiwe.â
3 Wakati huo makuhani wakuu na wazee wa watu walikutana pamoja katika ukumbi wa Kayafa, kuhani mkuu.
4 Wakashauriana jinsi ya kumtia Yesu nguvuni kwa hila wamuue.
5 Lakini wakaamua jambo hilo lisifanyike wakati wa sikukuu, kusije kukatokea ghasia kati ya watu.
Yesu anapakwa marashi Bethania
(Marko 14:3-9; Yoh 12:1-8)
6 Yesu alipokuwa Bethania, nyumbani kwa Simoni, aitwaye Mkoma,
7 mama mmoja aliyekuwa na chupa ya alabasta yenye marashi ya thamani kubwa, alimjia pale mezani alipokuwa amekaa kula chakula, akammiminia hayo marashi kichwani.
8 Wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, âYa nini hasara hii?
9 Marashi haya yangaliweza kuuzwa kwa bei kubwa, maskini wakapewa hizo fedha.â
10 Yesu alitambua mawazo yao, akawaambia, âMbona mnamsumbua huyu mama? Yeye amenitendea jambo jema.
11 Maskini mnao daima pamoja nanyi, lakini mimi sitakuwapo pamoja nanyi daima.
12 Huyu mama amenimiminia marashi ili kunitayarisha kwa maziko.
13 Nawaambieni kweli, popote ulimwenguni ambapo hii Habari Njema itahubiriwa, kitendo hiki alichofanya mama huyu kitatajwa kwa kumkumbuka yeye.â
Yuda anaamua kumsaliti Yesu
(Marko 14:10-11; Luka 22:3-6)
14 Kisha, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili, akaenda kwa makuhani wakuu,
15 akawaambia, âMtanipa kitu gani kama nikimkabidhi Yesu kwenu?â Wakamhesabia vipande thelathini vya fedha;
16 na tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta nafasi ya kumsaliti.
Maandalizi ya karamu ya Pasaka
(Marko 14:12-21; Luka 22:7-13,21-23; Yoh 13:21-30)
17 Siku ya kwanza kabla ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi walimwendea Yesu wakamwuliza, âUnataka tukuandalie wapi chakula cha Pasaka?â
18 Yeye akawajibu, âNendeni mjini kwa mwanamume fulani, mkamwambie: âMwalimu anasema, wakati wangu umefika; kwako nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu.ââ
19 Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaandaa Pasaka.
20 Kulipokuwa jioni, Yesu akakaa mezani pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili.
21 Walipokuwa wakila, Yesu akasema, âNawaambieni kweli, mmoja wenu atanisaliti.â
22 Wanafunzi wakahuzunika sana, wakaanza kuuliza mmojammoja, âBwana! Je, ni mimi?â
23 Yesu akajibu, âAnayechovya mkate pamoja nami katika bakuli ndiye atakayenisaliti.
24 Naam, Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yasemavyo, lakini ole wake mtu yule atakayemsaliti Mwana wa Mtu! Ingalikuwa afadhali kwa mtu huyo kama hangalizaliwa.â
25 Yuda, ambaye ndiye aliyetaka kumsaliti, akamwuliza, âMwalimu! Je, ni mimi?â Yesu akamjibu, âWewe umesema.â
Karamu ya Bwana
(Marko 14:22-26; Luka 22:14-20; 1Kor 11:23-25)
26 Walipokuwa wanakula, Yesu akatwaa mkate, akamshukuru Mungu, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, âTwaeni mle; huu ni mwili wangu.â
27 Kisha akatwaa kikombe cha divai, akashukuru, akawapa akisema, âKunyweni nyote;
28 maana hii ni damu yangu inayothibitisha agano, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi ili kuwaondolea dhambi.
29 Nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.â
30 Baada ya kuimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni.
Yesu anatangaza kwamba Petro atamkana
(Marko 14:27-31; Luka 22:31-34; Yoh 13:36-38)
31 Kisha Yesu akawaambia, âUsiku huu wa leo, nyinyi nyote mtakuwa na mashaka nami, maana Maandiko Matakatifu yasema: âNitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika.â
32 Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulieni Galilaya.â
33 Petro akamwambia Yesu, âHata kama wote watakuwa na mashaka nawe na kukuacha, mimi sitakuacha kamwe.â
34 Yesu akamwambia, âKweli nakuambia, usiku huu kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.â
35 Petro akamwambia, âHata kama ni lazima nife pamoja nawe, sitakukana kamwe.â Wale wanafunzi wengine wote wakasema vivyo hivyo.
Yesu anasali bustanini Gethsemane
(Marko 4:32-42; Luka 22:39-46)
36 Kisha Yesu akaenda pamoja nao bustanini Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, âKaeni hapa nami niende pale mbele kusali.â
37 Akawachukua Petro na wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuwa na huzuni na mahangaiko.
38 Hapo akawaambia, âNina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami.â
39 Basi, akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akasali: âBaba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki kinipite; lakini isiwe nitakavyo mimi, ila utakavyo wewe.â
40 Akawaendea wale wanafunzi, akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, âNdio kusema hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?
41 Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho inataka lakini mwili ni dhaifu.â
42 Akaenda tena mara ya pili akasali: âBaba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kipite bila mimi kukinywa, basi, utakalo lifanyike.â
43 Akawaendea tena, akawakuta wamelala, maana macho yao yalikuwa yamebanwa na usingizi.
44 Basi, akawaacha, akaenda tena kusali mara ya tatu kwa maneno yaleyale.
45 Kisha akawaendea wale wanafunzi, akawaambia, âJe, mngali mmelala na kupumzika? Tazameni! Saa yenyewe imefika, na Mwana wa Mtu atatolewa kwa watu wenye dhambi.
46 Amkeni; twendeni zetu. Tazameni! Anakuja yule atakayenisaliti.â
Yesu anatiwa nguvuni
(Marko 14:43-50; Luka 22:47-53; Yoh 18:3-12)
47 Basi, Yesu alipokuwa bado anasema nao, mara akaja Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili. Pamoja naye walikuja watu wengi wenye mapanga na marungu ambao walitumwa na makuhani wakuu na wazee wa watu.
48 Huyo aliyetaka kumsaliti Yesu, alikuwa amekwisha kuwapa ishara akisema: âYule nitakayembusu ndiye; mkamateni.â
49 Basi, Yuda akamkaribia Yesu, akamwambia, âShikamoo, Mwalimu!â Kisha akambusu.
50 Yesu akamwambia, âRafiki, fanya ulichokuja kufanya.â Hapo wale watu wakaja, wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni.
51 Mmoja wa wale waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono, akauchomoa upanga wake, akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.
52 Hapo Yesu akamwambia, âRudisha upanga wako alani, maana yeyote anayeutumia upanga, atakufa kwa upanga.
53 Je, hamjui kwamba ningeweza kumwomba Baba yangu naye mara angeniletea zaidi ya vikosi kumi na viwili vya malaika?
54 Lakini yatatimiaje Maandiko Matakatifu yasemayo kwamba ndivyo inavyopaswa kuwa?â
55 Wakati huohuo Yesu akauambia huo umati wa watu waliokuja kumtia nguvuni, âJe, mmekuja kunikamata kwa mapanga na marungu kana kwamba mimi ni mnyanganyi? Kila siku nilikuwa hekaluni nikifundisha, na hamkunikamata!
56 Lakini haya yote yametendeka ili maandiko ya manabii yatimie.â Kisha wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.
Yesu mbele ya baraza
(Marko 14:53-65; Luka 22:54-55,63-71; Yoh 18:13-14,19-24)
57 Basi, hao watu waliomkamata Yesu walimpeleka nyumbani kwa Kayafa, kuhani mkuu, walikokusanyika waalimu wa sheria na wazee.
58 Petro alimfuata kwa mbali mpaka uani kwa kuhani mkuu, akaingia ndani pamoja na walinzi ili apate kuona mambo yatakavyokuwa.
59 Basi, makuhani wakuu na Baraza lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu wapate kumuua,
60 lakini hawakupata ushahidi wowote, ingawa walikuja mashahidi wengi wa uongo. Mwishowe wakaja mashahidi wawili,
61 wakasema, âMtu huyu alisema: âNinaweza kuliharibu hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.ââ
62 Kuhani mkuu akasimama, akamwuliza Yesu, âJe, hujibu neno? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?â
63 Lakini Yesu akakaa kimya. Kuhani mkuu akamwambia, âNakuapisha kwa Mungu aliye hai, tuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu!â
64 Yesu akamwambia, âWewe umesema! Lakini nawaambieni, tangu sasa mtamwona Mwana wa Mtu ameketi upande wa kulia wa yule Bwana Mwenye Nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni.â
65 Hapo, kuhani mkuu akararua mavazi yake, akasema, âAmekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi? Sasa mmesikia kufuru yake.
66 Nyinyi mwaonaje?â Wao wakamjibu, âAnastahili kufa!â
67 Kisha wakamtemea mate usoni, wakampiga makofi. Wengine wakiwa wanampiga makofi,
68 wakasema, âTubashirie basi, wewe Kristo; ni nani amekupiga!â
Petro anamkana Yesu
(Marko 14:66-72; Luka 22:56-62; Yoh 18:15-18,25-27)
69 Petro alikuwa ameketi nje uani. Basi, mtumishi mmoja wa kike akamwendea, akasema, âWewe ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.â
70 Petro akakana mbele ya wote akisema, âSijui hata unasema nini.â
71 Alipokuwa akitoka mlangoni, mtumishi mwingine wa kike akamwona, akawaambia wale waliokuwa pale, âMtu huyu alikuwa pamoja na Yesu wa Nazareti.â
72 Petro akakana tena kwa kiapo: âSimjui mtu huyo.â
73 Baadaye kidogo, watu waliokuwa pale wakamwendea Petro, wakamwambia, âHakika, wewe pia ni mmoja wao, maana msemo wako unakutambulisha.â
74 Hapo Petro akaanza kujilaani na kuapa akisema, âSimjui mtu huyo!â Mara jogoo akawika.
75 Petro akakumbuka maneno aliyoambiwa na Yesu: âKabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.â Basi, akatoka nje, akalia sana.